MASOMO YA MISA
9 Januari, 2024
DOMENIKA YA 5 MWAKA c
SOMO LA KWANZA:Isa 6:1-2a, 3-8
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab 16:5,8-11
Bwana huishika kweli milele, Bwana ndiye fungu la posho langu, Wewe unaishika kura yangu. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini. Maana hutaiacha nafsi yangu kuzimu, Wala hutamto mtakatifu wako aone uharibifu. (K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. Utanijulisha njia ya uzima, Mbele ya uso wako ziko furaha tele. Na katika mkono wako wa kuume, Mna mema ya milele. (K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe.
SOMOLA PILI:1Kor 15:1-11
Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
Ufu 2:10
Aleluya, aleluya,
Aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu..
Aleluya
INJILI
Lk 5:1-11
Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata. .
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo.
Kwa masomo ya misa za kila siku, Sala mbalimbali na historia za maisha ya watakatifu tembelea catholickigomadiocese.org